Wasiliana nasi | FAQ | Mails | Malalamiko |

Tanga Regional Referral Hospital
(Bombo Hospital)

HUDUMA ZA UPASUAJI

Posted on: December 30th, 2024

I

Picha ya madakitari wakifamfanyia Upasuaji Mgonjwa

Idara ya Upasuaji ni miongoni mwa idara sita za kitabibu zinazotolewa katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga. Idara hii inafanywa na vitengo vitano ambavyo vimegawanywa kulingana na maeneo ya ubobezi/utaalamu. Vitengo hivi ni Upasuaji, Mifupa, Meno, Chumba cha Upasuaji, na Macho. Jukumu kuu la Idara ni kuhakikisha huduma sahihi za upasuaji na zilizo boreshwa zinatolewa kwa wagonja wote.

Kitengo cha Upasuaji

Kitengo hiki kinahusika na wagonjwa wote wanaohitaji upasuaji kwa magonjwa ya ndani, pua koo na masikio pamoja na urolojia. Pia inatoa huduma kwa wagonjwa wa dharura zinazosababishwa na ajali zinazopelekea kuumia sehemu ya kifua au tumbo. Miongoni mwa Huduma zisizo za dharura zinazotolewa ni Upasuaji wa Ngiri, magonjwa ya mfumo wa nyongo, matiti, nk. Pia tunatoa Huduma za upasuaji wa dharura kwa magonjwa kama vile upasuaji wa tumbo kutokana na maambukizi (peritonitis), kuziba kwa mfumo wa chakula (Intestinal Obstruction) na kuondoa sehemu ya mguu kutokana na madhara ya Kisukari(Diabetic foot) au mishipa ya damu(Gangrene). Baadhi ya upasuaji wa magonjwa ya Urolojia yanayofanyika ni pamoja na tezi dume, kurekebisha Kibofu cha mkojo kilichoumia, kuwekewa njia mbadala ya kukojolea (SPC) kutokana njia ya mkojo kuziba.

Kitengo kinaundwa na sehemu mbili wodi ya 7 (Kwa wanaume) na 9 (wanawake na watoto) ikiwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 51 kwa wakati mmoja. Timu ya watoa huduma inaundwa na Madaktari 2 Manesi 14 wakiongozwa na Madaktari bingwa 2.

Kitengo cha Upasuaji wa mifupa

Kitengo hiki kinajihusisha na magonjwa ya mifupa. Magonjwa ya dharura na yasiyo dharura ya mifupa. Miongoni mwa magonjwa yanayohitaji upasuaji wa dharura ni pamoja na Mivunjiko na mfupa nje ya kidonda (Open fracture), Kupoteza kiungo cha mwili katika ajali (Traumatic Amputation) pamoja na mteguko wa kiungo (dislocation). Baadhi ya huduma za upasuaji kwa magonjwa yasiyo ya dharura yanayotolewa na kitengo hiki ni kama vile Jipu la mfupa, mivunjiko ya mfupa ya aina mbalimbali, mivunjiko ya mifupa isiyounga au kuunga vibaya, magonjwa ya viungo ya kuzaliwa nk.

Kitengo kinaundwa na sehemu mbili wodi ya 8 (Kwa wanaume) na 9 (wanawake na watoto) ikiwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 51 kwa wakati mmoja. Timu ya watoa huduma inaundwa na madaktari katika mafunzo(interns) Madaktari 4 Manesi 10 wakiongozwa na Madaktari bingwa 3.

Kitengo Cha Macho

Kitengo cha macho ni moja kati ya vitengo  vitano vya idara ya Upasuaji katika hospital ya rufaa mkoani Tanga. Kitengo hiki kinatoa huduma kwa wagonjwa wa macho kwa Mkoa wa Tanga na maeneo jirani. Ugunduzi wa wagonjwa wa macho wanaohitaji upasuaji hufanyika katika kliniki zetu na hupangiwa utaratibu wa matibabu kulingana na udharura wa tatizo la mgonjwa. Kwa magonjwa ya dharura hufanyiwa upasuaji haraka iwezekanavyo. Wagonjwa hulazwa kupitia wodi  za vitengo vya upasuaji, mifupa au idara ya magonjwa ya ndani.

Huduma tunazotoa:

  • Uchunguzi wa Uoni
  • Utafiti/Uchunguzi wa kengeza
  • Uchunguzi wa sehemu ya jicho (ocular fundus)
  • Upasuaji wa mtoto wa jicho
  • Huduma za Mkoba

Chumba cha upasuaji:

Katika Hospitali yetu kitengo hiki kilikamilika mnamo mwaka 2006 kikilenga kuwezesha upatikanaji wa huduma za upasuaji. Kina jumla ya vyumba vitatu vya upasuaji, viwili kwaajili na kunawia, vyumba viwili vya kubadilishia nguo, stoo ya vifaa, ofisi mbili, chumba cha maandalizi na uangalizi baada ya upasuaji (recovery), chumba cha mapumziko na chumba cha kusafishia na kuchemshia vifaa vya upasuaji (sterilization). Kitengo hiki hutoa siku 2 kwa wiki kwa kila kitengo katika idara ya upasuaji. Chumba kimoja hutengwa kwaajili ya upasuaji wa dharura kwa wagonjwa kutoka kitengo chochote

Huduma tunazotoa:

  • Upasuaji Mkubwa
  • Upasuaji Mdogo
  • Chunguzi mbalimbali
  • Kusafisha na kuchemsha vifaa vya matibabu