Wasiliana nasi | FAQ | Mails | Malalamiko |

Tanga Regional Referral Hospital
(Bombo Hospital)

Ijue Saratani ya Kinywa

Posted on: October 21st, 2019

SARATANI YA KINYWA

Saratani ya kinywa ni ile saratani ambayo inatokea katika maeneo mbalimbali ya kinywa. Hivyo saratani hii huweza kutokea kwenye maeneo kama vile:

  • Midomo
  • Fizi
  • Ulimi
  • Sehemu za ndani za kinywa
  • Kaakaa
  • Sehemu ya kinywa iliyo chini ya ulimi

Saratani zinazotokea kinywani ni mojawapo ya saratani zilizomo katika makundi ya saratani zinazoathiri maeneo ya shingo na kichwa, na hata matibabu yake huwa sawa kwa kiwango fulani.

DALILI ZAKE

  • Dalili na alama za saratani ya kinywa huweza kuwa zifuatazo:
  • Kidonda kisichopona
  • Kidonda ambacho kinatoa damu kikiguswa kidogo tu
  • Kuota kwa kitu kipya kinywani, ama uvimbe katika sehemu yeyote ya kinywa
  • Maumivu makali ya ulimi
  • Kushindwa kutafuna ama kuwa na maumivu wakati wa kutafuna
  • Kuwa na maumivu wakati wa kumeza chakula

NI WAKATI GANI UMUONE DAKTARI

Ni vizuri kumuona daktari mara tu uonapo mojawapo ya dalili hizo kinywani ambazo zipo kwa zaidi ya wiki mbili. Daktari ataweza kufanya uchunguzi kulingana na dalili zake, na pia kumuwezesha daktari kutofautisha kati ya maambukizi yanayoweza kuwa na dalili kama hizo wakati si saratani.

SABABU ZA KUTOKEA KWA SARATANI 

Saratani kwenye kinywa hutokea wakati chembe hai(cell) zilizoko kinywani na maeneo yote ya kinywa  zinapopata mabadiliko kwenye vinasaba vyake (DNA). Mabadiliko haya husababisha chembe hai hizi kuzaliana na kukua nje ya utaratibu na wakati huohuo chembe hai zilizo na afya kufa. Ni mkusanyiko huu wa chembe hai ndio unapelekea kutokea kwa saratani husika. Kadiri muda unavyokwenda ndivyo ambavyo saratani huweza kusambaa katika maeneo mengine ya mwili kama vile shingoni, n.k.

Kitaalam bado haijulikani ni nini hasa kinachopelekea mabadiliko haya kwenye chembe hai hizi na hivyo kuvuruga utaratibu wake wa kuzaliana, na hivyo kupelekea kutokea kwa saratani. Hata hivyo madaktari wanatambua vitu ambavyo ni hatarishi na ambavyo vinaweza kuchangia kusababisha mabadiliko kwenye chembe hai hizi na hivyo kupelekea saratani.

SABABU HATARISHI

Zifuatazo ni mojawapo ya sababu hatarishi kwa kusababisha saratani kinywani:

  • Matumizi yeyote ya tumbaku kama vile sigara, ugoro nk
  • Matumizi ya vileo
  • Midomo kupigwa na jua kwa muda mrefu
  • Kupata maambukizi ya virusi kinywani
  • Kuwa na kinga dhafu

NAMNA YA KUJUA UGONJWA HUU

Saratani ya kinywa huweza kujulikana kitaalam baada ya kufanya uchunguzi kwa namna mbalimbali ikiwemo zifuatazo:

  • Uchunguzi wa kawaida. Daktari wa kawaida ama wa kinywa na meno anaweza kuangalia kinywani ili kuona kitu ambacho umemuelezea ili kujua kitaalamu ni nini.
  • Kufanya Uchunguzi wa kimaabara. Kama itaonekana ni kitu ambacho kinahitaji uchunguzi zaidi inaweza kushauriwa kufanyika kwa uchunguzi wa kimaabara ambapo sehemu ndogo ya eneo huchukuliwa kitaalam na kupelekwa maabara kwa uchunguzi zaidi. 

MATIBABU

Matibabu ya saratani hutegemea mahali hiyo saratani ilipo na iko kwenye hatua gani katika kuendelea kwako kushambulia mwili, hali ya jumla ya kiafya ya muhusika na pia mapendekezo ya mtu binafsi. Hivyo basi inawezekana kabisa ukawa na matibabu ya mara moja ama ukawa na mchanganyiko wa matibabu kulingana na vigezo nilivyovitaja hapo juu. Matibabu ya saratani yamegawanyika katika makundi yafuatayo

  • Upasuaji
  • Mionzi
  • Madawa

Hivyo ni vizuri kujadiliana na daktari ama jopo la madaktari wanaomtibu mgonjwa wa saratani ili kueleweshana na kukubaliana juu ya matibabu ya mgonjwa. 

UPASUAJI

Matibabu ya upasuaji kwenye saratani ya kinywa umegawanyika katika makundi yafuatayo;

  • Upasuaji kuondoa uvimbe. Katika upasuaji huu daktari anaweza kukata uvimbe wote na baadhi ya sehemu ambazo hazijafikiwa na uvimbe bado ili kujiridhisha kwamba chembe hai zote zenye saratani zimeondolewa. Saratani ambazo ni ndogo huweza kuondolewa kwa upasuaji mdogo, wakati saratani kubwa huhitaji upasuaji mkubwa zaidi, ambapo huweza kuhusisha hata sehemu za mfupa wa taya ama ulimi nk.
  • Upasuaji wa kuondoa saratani liyosambaa mpaka shingoni. Inapothibitika kuwa saratani iliyoanzia kinywani imesambaa mpaka kwenye maeneo ya shingo, ukubwa wa eneo la upasuaji huongezeka na kufikia maeneo ya shingo ili kuhakikisha kwamba sehemu zote zilizoathiriwa na saratani zinaondolewa na hivyo kuondoa uwezekano wa saratani kubaki na kisha kuanza tena kukua.

Upasuaji kwenye maeneo ya kinywa huweza kuathiri namna unavyoonekana na hata wakati mwingine hata uwezo wako wa kuongea, kula na kumeza chakula huweza kuathirika.

MATIBABU YA MIONZI

Mionzi hutumika kuua chembe hai ambazo zina saratani, matibabu ya mionzi pekee hutumika pale tu inapothibitika kuwa saratani yako iko kwenye hatua za awali. Halikadhalika mionzi huweza kutumika kama nyongeza baada ya upasuaji. Pia wakati mwingine mionzi huweza kuunganishwa na madawa anayopewa mgonjwa.

MADHARA YA MIONZI

Madhara yatokanayo na mionzi ni pamoja na yafuatayo kinywa kuwa kikavu, meno kuoza, kuharibika kwa mfupa wa taya, kutokea kwa vidonda kinywani, fizi kutoa damu, ngozi kuwa nyekundu kama iliyoungua.

Hivyo daktari ama jopo la madaktari wanaomtibu mgonjwa wa saratani ya kinywa hushauri mgonjwa kumuona daktari wa kinywa na meno kama ya kuanza matibabu ya mionzi ili kujiridhisha kwamba afya yako ya kinywa iko vizuri na kama kuna matibabu basi yaanze kufanyika kwanza kabla ya kuanza kwa mionzi

MATIBABU YA MADAWA

Haya ni madawa ambayo hutumika kuua chembe hai zilizo na saratani mwilini. Madawa haya huweza kutumika peke yake ama yakiwa yameunganishwa na matibabu mengine kama vile mionzi. Kwa kua mara nyingi madawa haya huongeza ufanisi wa mionzi, hivyo mara nyingi huunganishwa pamoja.

MADHARA YATOKANAYO NA MIONZI

Madhara yatokanayo na matumizi ya madawa haya kwenye matibabu ya saratani hutofautiana kutegemea na aina ya dawa unayotumia. Hata hivyo madhara ambayo mara nyingi huwapata Watumiaji wa madawa haya ni Kichefuchefu, kutapika na kunyonyoka kwa nywele.


Maoni, maswali na Ushauri fika Hospitali iliyo jirani upate ufafanuzi zaidi