Wasiliana nasi | FAQ | Mails | Malalamiko |

Tanga Regional Referral Hospital
(Bombo Hospital)

Meno Kulegea na Kung’oka Yenyewe

Posted on: October 18th, 2019

Meno Kulegea Na Hata Kung’oka Yenyewe

(Periodontitis)

Ni watu wengi hasa wa kuanzia umri wa kati na kuendelea hupatwa na hali hii ya kuwa na meno yanayolegea na wanapoyachunguza hukuta meno husika hayana matundu na hali hii ya meno kulegea haiambatani na maumivu yeyote kwenye meno husika  ama kinywani kwa ujumla wake. Kwa makundi mengine meno haya yaliyolegea huweza pia kung’oka kirahisi wanapong’atia kitu. Huu ni ugonjwa unaoathiri mfupa wa taya lililoshikilia meno husika, hivyo basi sehemu husika za mfupa wa taya ambazo hushikilia meno zinazoshambulia na ugonjwa huu huwa dhaifu na kipenyo chake kutanuka, mara kipenyo chake ambamo jino hujishika kinapotanuka jino husika huweza kulegea, kitaalamu ugonjwa huu huitwa Periodontitis.

Dalili Za Ugonjwa Huu

Zifuatazo ni baadhi ya dalili za ugonjwa huu, zingatia kwamba si lazima mtu mmoja awe na dalili zote hizi:

  • Fizi kujivuta kutoka kwenye meno na hivyo kuyafanya meno yaonekane ni marefu kuliko kawaida yake kabla ya ugonjwa huu
  • Meno kuachana na kutengeneza nafasi mpya katika meno yako ambazo hazikuwepo hapo kabla( mianya ya ukubwani)
  • Kutoka usaha kati ya meno yako na fizi
  • Meno yaliyolegea
  • Mabadiliko ya mpangilio wako wa meno

Ni Lini Umuone Daktari wa Kinywa Na Meno

Fizi zilizo na afya njema huwa ni ngumu zinapobonyezwa na pia zina rangi ya pinki iliyopauka. Hivyo kama fizi zako ni nyekundu, zinabonyea na kutoa damu kiurahisi, ama una moja ama zaidi ya dalili zilizotajwa hapo juu za ugonjwa huu, ni vema ukamuona daktari mapema. Kadiri unavyochukua uamuzi wa kumuona daktari mapema ndivyo unavyokua na nafasi nzuri zaidi ya kurekebisha uharibifu unaosababishwa na ugonjwa huu, halikadhalika kuzuia magonjwa mengine ambayo huweza kutokea kutokana na kuwepo kwa ugonjwa huu wa fizi uliokamaa (Periodontitis).

Sababu Za Ugonjwa Huu

Kwa watu wengi wanapojichunguza meno yao huona kuna tabaka fulani gumu ambalo huwa limejijenga kwenye meno yao katika eneo ambalo jino hukutana na ufizi, kwa meno ya chini mara nyingi huwa ni kwa ndani ambapo meno hutazamana na ulimi lakini kwa meno ya juu tabaka hili gumu huweza kutokea pande zote. Kitaalamu tabaka hili gumu huitwa ugaga na huwa haiwezekani uwezi kuondoa ugaga kwa kupiga mswaki ama kwa kufanya flosi badala yake unahitajika kufanyiwa usafi kitaalam ili kuundoa.

Kadiri tabaka laini na ugaga vinapokaa kwa muda mrefu kwenye meno yako, ndivyo hivyo huweza kuleta madhara. Mwanzoni huweza tu kufanya fizi zivimbe na kutoa damu unapopiga mswaki. Mwendelezo wa fizi kuvimba hupelekea kutengeneza kwa nafasi katika meno yako (pockets) ambazo pia hukaliwa na bakteria, tabaka laini na ugaga. Kadiri bakteria hawa wanapoendelea kuishi kwenye sehemu husika hutoa sumu (endotoxin) ambayo huhusika moja kwa moja na kuendelea kwa ugonjwa huu. Kadiri muda unavyokwenda ndivyo nafasi hizi huzidi kukua na kufika mfupa ulioshikilia jino ambao nao unaposhambuliwa huwa dhaifu na kushindwa kuendelea kushikilia jino ambalo baadae hulegea na hata kung’oka.

Sababu Hatarishi

Zifuatazo ni sababu ambazo uwepo wake kwa mtu huongeza uwezekano wa mtu husika kupata ugonjwa huu:

  1. Tabia za usafi wa kinywa zisizoridhisha
  2. Matumizi ya tumbaku
  3. Kisukari
  4. Uzee
  5. Kupungua  kwa kinga ya mwili kunakotokana na sababu mbalimbali kama vile VVU/Ukimwi nk

Madhara Zaidi (Complications)

Baadhi ya madhara ya ugonjwa huu ni yafuatayo:

  1. Kupoteza meno
  2. Kutokea kwa jipu na maumivu makali

Matibabu

Matibabu ya ugonjwa huu hulenga kusafisha meno na maeneo yanayozunguka meno pamoja na nafasi zilizojitengeneza (Pockets), ili kuondoa ugaga. Usafi huu hufanywa na daktari kwa vifaa maalumu hospitalini. Unapofanyiwa matibabu haya una nafasi nzuri ya kupona kama tu utazingatia namna bora ya kuhakikisha unafanya usafi wa kinywa vizuri na hivyo kuhakikisha kinywa na kisafi muda wote.

Mitindo ya maisha na matibabu binafsi

  • Fanya yafuatayo ili kujiepusha na ugonjwa huu:
  1. Fanya usafi wa kinywa kama inavyoshauriwa na daktari wako.
  2. Tumia mswaki ambao unaubadilisha kila baada ya miezi mitatu.
  3. Hakikisha unapiga mswaki mara mbili kwa siku asubuhi baada ya kula na usiku kbla ya kulala.
  4. Fanya flosi kila siku.
  5. Tumia dawa za kusukutua ili kusaidia kupunguza tabaka laini kwenye meno yako.

Kuzuia

  • Namna bora zaidi ya kuzuia ugonjwa huu ni kuanza kufanya na kufuatisha masharti ya usafi wa kinywa mapema kabisa katika maisha yako na kutoacha kamwe maishani mwako. Hii ikiwa na maana kupiga mswaki mara mbili kwa siku asubuhi na jioni na kufanya flosi mara moja kwa siku.
  • Muone daktari wa kinywa na meno mara kwa mara, na hasa mara moja kila baada ya miezi sita. Hata hivyo kama daktari wako ataona uko kwenye mazingira hatarishi zaidi anaweza kukupangia utaratibu wa kumuona mara nyingi zaidi

Maoni, Maswali na Ushauri: Fika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Kitengo cha Afya ya Kinywa na Meno upate majibu sahihi kwa Afya Yako