Wasiliana nasi | FAQ | Mails | Malalamiko |

Tanga Regional Referral Hospital
(Bombo Hospital)

YAS YAKABIDHI VIFAA TIBA KWA HOSPITALI YA BOMBO.

Posted on: June 12th, 2025



Kampuni ya Mawasiliano ya YAS zamani Tigo imekabidhi vifaa tiba kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo mapema leo Juni 13,2025 ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii na kutambua mchango wa Serikali katika kudumisha huduma za afya nchini.

Akizungumza mara baada ya kupokea vifaa tiba hivyo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Bombo Dkt. Frank Shega amesema " Tunaishukuru Kampuni ya YAS kwa mchango wao katika Hospitali yetu kwani wametusaidia vifaa tiba ikiwemo vitanda vya kujifungulia, vifaa maalum vya kusikilizia mapigo ya moyo kwa mama mjamzito,vitanda vya kulalia pamoja na mashuka; kwahiyo vifaa hivi tulivyokabidhiwa leo na Kampuni ya YAS vinakwenda kutusaidia kwa ukubwa katika Hospitali yetu kwasababu Hospitali hii inahudumia halmashauri zote 11 za Mkoa wa Tanga pamoja na kusaidia wagonjwa wanaokuja mahali hapa kupata huduma".

"Aidha niwaombe na wadau taasisi nyingine kuiga mfano kwa Kampuni ya YAS katika kurudisha kwa jamii ili kusaidia kasi katika kutoa huduma bora za afya ".

Pia, Bw. Abdul Ally ambaye ni Mkurugenzi wa YAS Kanda ya Pwani Kaskazini amesema "Sisi kama Kampuni tunafahamu kulingana na programu za Wizara ya Afya kati ya wanawake 5-10 wanakutana na changamoto mbalimbali wakati wa kujifungua, hivyo tumelitambua hilo na tumeamua kurudisha kwa jamii kwa kukabidhi vifaa tiba hivi kwa Hospitali ya Bombo ikiwa pia ni sehemu ya kuiunganisha Kampuni ya YAS pamoja na jamii".