WAZIRI MHAGAMA: SERIKALI YA AWAMU YA SITA KUFANYA MABORESHO KUBADILI MUONEKANO WA HOSPITALI YA BOMBO.
Posted on: February 27th, 2025
WAZIRI MHAGAMA: SERIKALI YA AWAMU YA SITA KUFANYA MABORESHO KUBADILI MUONEKANO WA HOSPITALI YA BOMBO.
Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuanza Ujenzi na Ukarabati wa majengo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo kwa kuanza ujenzi Jengo la Wodi ya Mama na Mtoto ifikapo mwezi wa tano ili kurahisisha upatikanaji wa Huduma za Uzazi kwa Mama na Mtoto.
Ameyasema hayo Jenista Mhagama Waziri wa Afya mapema leo Februari 27,2025 wakati akiongoza mamia ya wanawake wa CCM waliojitokeza katika Viwanja vya Urithi vilivyopo Jijini Tanga kwa ajili ya kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu kwa utendaji kazi wake wa kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini. Ikumbukwe kuwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ameweka kambi katika Mkoa wa Tanga kwa ziara ya wiki moja kutembelea miradi mbalimbali katika Halmashauri za Mkoa wa Tanga.
"Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu imeweka takribani Bilioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto pamoja na Ukarabati wa Majengo ya Mwapachu na Sokoine ambapo kiasi cha shilingi milioni 900 zimetengwa kwa ajili ya Ukarabati wa majengo hayo kwasababu tunataka Hospitali yetu ya Bombo ifanane na Serikali ya awamu ya Sita ".
"Katika kuonyesha kujali na kuthamini Sekta ya Afya nchini Serikali imejenga jumla ya vituo vya Afya 1044 nchi nzima na Hospitali 9 za wilaya katika Mkoa huu wa Tanga huku nyingine zikiwa ni mpya na nyingine zimekarabatiwa na tuwaambie tu kuwa hatutalala hadi pale tutakapohakikisha Sekta ya nchini ipo sawasawa".
Mhe. Mhagama amesema "85% ya Watanzania wanapata huduma za afya kwa umbali usiozidi kilomita 5 huku wajawazito takribani milioni 3 nchini wameweza kuhudhuria kliniki angalau mara 4 bila kukosa kutokana na kuvutiwa na Vituo vya Afya vilivyopo kila kona ya nchi na kupelekea kupunguza idadi ya vifo kutoka 67 kwa vizazi hai 1000 hadi vifo 43 kwa vizazi hai 1000 ".
Aidha, katika hafla hiyo huduma kadhaa zimetolewa kwa wananchi waliojitokeza Viwanjani hapo ikiwemo zoezi la uchangiaji damu lililoratibiwa na Mpango wa Taifa wa damu salama kwa kushirikiana na Hospitali ya Bombo pamoja na Halmashauri ya Jiji la Tanga.