WATUMISHI BOMBO WAPATIWA MAFUNZO YA MAADILI,SHERIA NA TARATIBU ZA UTUMISHI WA UMMA
Posted on: March 9th, 2025
WATUMISHI BOMBO WAPATIWA MAFUNZO YA MAADILI,SHERIA NA TARATIBU ZA UTUMISHI WA UMMA
Watumishi kutoka Idara na vitengo mbalimbali wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo wamepatiwa mafunzo ya awali ya Utumishi wa Umma kwa lengo la kuwaongezea ari na kuwaweka tayari kwa ajili ya kufanya kazi kwa uadilifu, bidii, weledi, uwajibikaji na ufanisi.
Mafunzo hayo ya siku tatu yemetolewa mapema siku ya leo Machi 10,2025 na wakufunzi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Singida kwa kushirikiana na Menejimenti ya Hospitali ya Bombo ambapo wamejifunza mambo mbalimbali ikiwamo maadili ya utumishi wa umma.
Akifungua mafunzo hayo Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Frank Shega amewataka watumishi hao kuwa makini kufuatilia mafunzo hayo ili kupata uelewa wa mafunzo hayo pamoja na kuzingatia taaluma zao na uadilifu kazini ili kuiwezesha Taasisi kufikia malengo iliyojiwekea.
"Mafunzo haya ni nyenzo muhimu ya upimaji wa utendaji wa watumishi wa umma kwenye taasisi za Serikali, hivyo natoa rai kwa watumishi kuzingatia mafunzo haya ili kuweza kuelewa sheria,kanuni,taratibu na miongozo ya utumishi wa umma hususani katika kutoa huduma kwa wateja wetu". Amesema Dkt. Shega.
Watumishi zaidi ya 100 wa kada mbalimbali ikiwamo Madaktari, wauguzi,watunza kumbukumbu, madereva, wataalamu wa maabara na TEHAMA wamepatiwa mafunzo hayo ambayo yamefanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Afya Bombo, Jijini Tanga huku jumla ya watumishi 540 wakitarajiwa kunufaika na mafunzo.