WATARAJALI BOMBO WAKUMBUSHWA MAADILI WAKATI WA KUTOA HUDUMA.
Posted on: November 25th, 2024WATARAJALI BOMBO WAKUMBUSHWA MAADILI WAKATI WA KUTOA HUDUMA.
Watumishi wa afya watarajali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo wameaswa kufuata maadili sahihi ya taaluma zao wakati wa kutoa huduma kwa wateja wanaofika Hospitalini hapa
Hayo yamesemwa mapema leo Novemba 26, 2024 na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Frank Shega wakati wa kuwajengea uelewa wataalam mbalimbali wakiwemo Madaktari, wauguzi, wafamasia na wataalam wa Maabara ambao wameanza mafunzo kwa vitendo Hospitalini hapa.
Amesema katika sekta ya afya kuna maeneo mawili ambayo mtoa huduma anapaswa kufahamu kwanza kabisa nidhamu kazini, lakini pia usiri kwa wagonjwa juu ya vipimo mnavyo vichukua mhakikishe majibu yake yanakua siri kati ya mteja na mtoa huduma.
“Baadhi ya watu mmekuwa na tabia za ajabu sana kwenye maeneo yenu ya kazi utakuta mgonjwa anakuja kupatiwa matibabu halafu baadae utamkuta mtu wa maabara anaanza kutoa siri za vipimo vya wagonjwa hilo suala sio la misingi ya taaluma ya kada za Afya”.
”ifikie kipindi jamii ifurahie na huduma mnayo itoa pindi mkiwa katika maeneo yenu ya kazi kwani maadili ya kazi ndiyo huleta matumaini kwa wagonjwa mnao wahudumia mfano mzuri nyie wenye taaluma nyeti ya vipimo maana mgojwa kabla ya kupata matibabu lazima apitie kwenu ili kufahamu njia gani mtaitumia kumsaidia”. Amesema Dkt. Shega
Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo kwa Vitendo kwa watarajali Hospitalini hapa Dkt. Joshua Jackson amesema "Nawasihi watarajali wote kufuata miiko na Sheria za Baraza la Madaktari kama zilivyoainishwa kwani kufanya vitendo ambavyo ni kinyume na taaluma vitasababisha kukosa vigezo vya wewe kuwa mtarajali".
“Kwahiyo onyesheni ushirikiano kwa wakuu wenu mkiwa wodini na kufuata utaratibu pale inapotokea changamoto kwa watarajali pindi wakiwa kwenye mafunzo hayo na sisi kwa nafasi zetu pamoja na Uongozi wa Hospitali nzima tutahakikisha tunatatua changamoto hizo ili kuendelea kutoa huduma bora ya Afya Hospitalini hapa".