Wasiliana nasi | FAQ | Mails | Malalamiko |

Tanga Regional Referral Hospital
(Bombo Hospital)

WARATIBU WA M-MAMA MKOA WA TANGA WAPATIWA MAFUNZO KUIELIMISHA JAMII UMUHIMU WA KUPIGA NAMBA 115.

Posted on: July 12th, 2024

WARATIBU WA M-MAMA MKOA WA TANGA WAPATIWA MAFUNZO KUIELIMISHA JAMII UMUHIMU WA KUPIGA NAMBA 115.

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi pamoja Shirika lisilo la Kiserikali la Pathfinder mapema leo Ijumaa ya Julai 12,2024 wametoa Mafunzo ya siku moja kwa Maafisa Habari, waelimisha umma pamoja na Waratibu wa mfumo wa m-mama ngazi ya Mkoa na Halmashauri katika Mkoa wa Tanga jinsi ya kuelimisha Jamii kuhusu Mfumo wa m-mama wa Rufaa zitakazotoka katika ngazi ya jamii kwenda kwenye vituo vya Afya pamoja na matumizi ya kupiga namba ya bure 115.

Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Regal Naivera Complex uliopo Jijini Tanga ambapo Afisa Habari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Afisa Habari wa Mkoa, Waelimisha umma na Waratibu wa Mfumo wa m-mama katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri wametakiwa kushirikiana na Waratibu wa m-mama Mkoa wa Tanga katika kuielimisha jamii juu ya mfumo wa m-mama na matumizi ya namba ya bure 115 pale inapotokea Dharura ya haraka kwa Mama Mjamzito,Mama aliyejfungua ndani ya siku 42 na mtoto Mchanga aliye ndani ya siku 28.

James Mhilu kutoka Wizara ya Afya ndiye Mkufunzi aliyeongoza Mafunzo hayo akisema kuwa, namba 115 ni namba maalum ambayo Wananchi wanatakiwa kuendelea kuitumia kwa kupiga simu Bure pale inapotokea Dharura kwa Mama Mjamzito ili aweze kupatiwa huduma ya usafiri kwa haraka na kuwahishwa katika kituo Cha Afya kilichopo karibu yake kupitia usafiri wa Gari za Madereva Jamii pasipo kutozwa kiasi chochote cha pesa kama ada ya huduma ya usafiri huo.

Aidha, kupitia Mafunzo hayo wadau walioshiriki kwa pamoja waliweza kuandaa Mpango kazi wa Mkoa wenye lengo la kuwafundisha na kuwaelimisha viongozi wa Ngazi zote kwenye jamii pamoja na wananchi ili kuwa na uelewa wa kutosha juu ya matumizi ya nambari 115.