RC BURIANI: RAIS AMEFANYA UWEKEZAJI MKUBWA KATIKA SEKTA YA AFYA
Posted on: May 2nd, 2024RC BURIANI: RAIS AMEFANYA UWEKEZAJI MKUBWA KATIKA SEKTA YA AFYA.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt.Batilda Buriani leo Mei 03,2024 amefunga rasmi Kambi ya Matibabu ya Madaktari Bingwa na Mabingwa wabobezi wa Dkt. Samia Kanda ya Kaskazini iliyokuwa ikiendelea hapa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga tangu tarehe 29,Aprili ambapo Kambi hiyo ilizinduliwa.
Katika hafla hiyo fupi Dkt. Batilda amesema “Tunamshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika Sekta ya Afya ambapo takribani trilioni 6.1 imewekezwa katika Sekta ya Afya pekee nchini. Tanga tulikuwa na Hospitali 2 tu za Wilaya sasa tunazo 6 mpya katika ngazi ya Wilaya na zina vitendea kazi vyote muhimu haswa katika upasuaji na kila kitu”.
“Tumeongeza Vituo vya Afya na Zahanati; kikubwa tunachokifanya kwa sasa kama Mkoa ni kuongeza jitihada katika Huduma ili tusiwe na malalamiko katika huduma zetu. Kama nyinyi watu 85 mmeweza kuhudumia wagonjwa 2536 kwa siku hizo 5 kwa maana mmehudumia watu 500 kwa siku ni idadi kubwa hivyo tunawashukuru kwa uchapakazi wenu na uzalendo wenu”.
Aidha, Dkt. Buriani ameiasa jamii kuhusu kubadili mitindo ya maisha yetu “Naomba nitumie fursa hii kwa kila mmoja wetu kubadili mtindo wetu wa maisha ya kila siku kuhusu matumizi ya sukari, mafuta na vyakula vya viwandani badala yake tutumie vyakula vyetu vya asili. Tuna viungo vyetu vya asili kama tangawizi na vingine ambavyo vinasaidia kutukinga na magonjwa mbalimbali, lakini pia tufanye mazoezi ya kukimbia au kutembea kwa maana yanasaidia katika kuimarisha Afya zetu.