Wasiliana nasi | FAQ | Mails | Malalamiko |

Tanga Regional Referral Hospital
(Bombo Hospital)

MBUNGE UMMY AKABIDHI AMBULANCE TANGA RRH

Posted on: July 26th, 2024

Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Mhe. Ummy Mwalimu ambaye pia ni Waziri wa Afya nchini amekabidhi gari maalumu la kubebea wagonjwa ‘ Ambulance’ ambalo litatumika kutoa huduma kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo.

Waziri Ummy amekabidhi Ambulance hiyo leo Jumamosi Julai, 27,2024 katika Viwanja vya Hospitali hiyo na kushuhudiwa na wananchi, Wataalam wa Afya Hospitalini humo, Mganga Mfawidhi pamoja Mganga Mkuu wa Mkoa.

Amesema hiyo ni Ambulance ya tatu kwa Jiji la Tanga ambayo ameitoa katika ahadi zake, ambapo iliyopita aliitoa katika Hospitali ya Wilaya iliyopo Masiwani, na leo amekabidhi Ambulance nyingine ili kuendelea kuboresha huduma za Afya.

"Nimekuja kwa awamu nyingine kukabidhi gari hili ‘Ambulance’ niliyopewa na Mama, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ili lisaidie kuboresha huduma za afya katika Jiji la Tanga. Ambulance ambayo naikabidhi leo itatumika kutoa huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga" amesema Ummy.

Aidha katika hafla hiyo Waziri Ummy Mwalimu amepiga marufuku kwa Hospitali zote nchini kuwatoza wananchi pesa ya posho ya Dereva wala Muuguzi anayemsindikiza Mgonjwa na badala yake Mwananchi atagharamia mafuta tu na sio vinginevyo.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo (MOI'c) Dkt.Frank Shega ameshukuru kupata Ambulance hiyo na kwamba sasa zimefika 2 katika Hospitali hiyo ambazo zitasaidia kubeba wagonjwa na kuwawahisha kupata huduma za matibabu.