Wasiliana nasi | FAQ | Mails | Malalamiko |

Tanga Regional Referral Hospital
(Bombo Hospital)

MAT TANGA KWA KUSHIRIKIANA NA GIFT OF HOPE FOUNDATION WAGAWA KADI ZA BIMA YA AFYA 20 KWA WAATHIRIKA WA DAWA ZA KULEVYA

Posted on: August 4th, 2024

MAT TANGA KWA KUSHIRIKIANA NA GIFT OF HOPE FOUNDATION WAGAWA KADI ZA BIMA YA AFYA 20 KWA WAATHIRIKA WA DAWA ZA KULEVYA.

Kitengo cha Methadone (MAT) kilichopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Gift of Hope Foundation wa Jijini Tanga mapema leo Agosti 7,2024 wamegawa kadi za Bima ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF iliyoboreshwa) kwa waraibu 20 ili kuwasaidia kupata matibabu katika Vituo vya Afya, Zahanati na Hospitali za Wilaya. Katika hafla hiyo fupi iliyofanyika kwenye Jengo la MAT-Bombo imehudhuriwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt.Frank Shega, Mkurugenzi wa Gift of Hope Foundation Ndg.Said Bandawe,Mkuu wa Kitengo cha Methadone Dkt. Wallace Karata pamoja na wataalam wengine Hospitalini hapo.

Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Frank Shega amewaasa wanufaika hao kutumia kadi hizo vizuri pamoja na kuzitunza kwa kuziweka mahali salama ili kurahisisha upewaji wa huduma pindi itakapohitajika. "Na sisi tuliopata kadi hizi za Bima tuzitunze zisipotee ili zitusaidie wakati wa uhitaji wa huduma za afya na pia kuwa na uhakika wa matibabu”.

“Pia nichukue fursa hii kuwashukuru Taasisi ya Gift of Hope Foundation katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika mchakato wa Bima ya Afya kwa wote na kuwaomba tuendelee kuweka mikakati zaidi katika kulinda afya zetu kwa kuhakikisha tunapata Bima za Afya zaidi ili kurahisisha kupata huduma za matibabu hadi kwenye ngazi ya Hospitali za Wilaya ” amesema Dkt. Shega.

Aidha, ameendelea kuipongeza Taasisi ya Gift of Hope Foundation chini ya Mkurugenzi wake Ndg. Said Bandawe kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha wanaungana na Serikali kutokomeza matumizi ya Dawa za Kulevya kwa kutoa elimu kwa Jamii na kuwakwamua Vijana ambao wamekuwa waraibu wa dawa za kulevya pamoja na kujitoa kwao ikiwemo kutoa kadi za Bima ya Afya kwa waraibu hao zinazokwenda kuwasaidia wao na familia zao kwa kwani kadi moja ya Bima ya Afya inaweza kuwahudumia watu watano kwenye kaya moja.

“Mwisho kabisa hongereni watumishi wote kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya na tuendelee kushirikiana kwa kufuata utaratibu kuwasilisha changamoto kwa Menejimenti na sisi tuko tayari kuzifanyia kazi ili kuendelea kuwahudumia wananchi wetu".