HOSPITALI YA RUFAA YA BOMBO YAPOKEA MAJERUHI WANNE MMOJA AKIWA AMEFARIKI
Posted on: January 25th, 2024
Na Oscar Assenga,Tanga.
HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga -Bombo imethibitisha kupokea majeruhi wanne kutoka Hospitali ya wilaya ya Muheza ambapo mmoja alipofika akiwa ameshapoteza uhai na mwengine alipata matibabu lakini ndani ya dakika tatu naye akawa amepoteza uhai kutokana na kuwa na majeraha makubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Hospitalini hapo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga -Bombo Dkt Frank Shega alisema majira ya mchana waliweza kupata taarifa za tukio la ajali hiyo ambayo ilitokea eneo la Mamboleo na Kwafungo
Alisema katika majeruhi wengine wawili waliobaki mmoja amepelekwa chumba cha upasuaji mpaka sasa anaendelea na madaktari wanaendelea kumpigania ili aweze kutoka salama.
Aidha alisema mwengine wa nne aliweza kupata majeraha makubwa sehemu mbalimbali za mwili hasa miguu kwa hiyo baada ya kufanyiwa uchunguzi madaktari bingwa kuangalia hali yake wameona ni vema aweze kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.
“Huyu aliyepelekwa chumba cha upasuaji changamopto kubwa amepata majeraha maeneo ya tumbo baada ya kumpokea na kumfanyia uchunguzi wa awali ikaonekana maeneo hayo amepata madhara makubwa kwa hiyo ikaonekana vi vema aingie huko kwa ajili ya kurekebisha changamoto zilizojitokeza eneo la tumbo hasa kwa ndani hivyo madaktari wanaendelea kumpatia matibabu”Alisema