Wasiliana nasi | FAQ | Mails | Malalamiko |

Tanga Regional Referral Hospital
(Bombo Hospital)

DKT.CAROLINE: SERIKALI IMEFANYA UWEKEZAJI MKUBWA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA.

Posted on: May 1st, 2024

DKT.CAROLINE: SERIKALI IMEFANYA UWEKEZAJI MKUBWA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA.

Mapema leo Mei 02,2024 Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tiba Wizara ya Afya Dkt. Caroline Damian ametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo kuangalia utekelezaji na uendeshaji wa Kambi ya Matibabu ya Madaktari Bingwa na Bingwa bobezi wa Dkt Samia Kanda ya Kaskazini waliokita kambi hapo kuanzia ile siku ya Jumatatu ya Aprili 29,2024.

Dkt. Caroline amesema”Wizara imeandaa kambi hizi maalum ili kuboresha utoaji wa huduma za Kibingwa na Ubingwa bobezi katika Hospitali za Mikoa karibu kabisa na wananchi. Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia imefanya uwekezaji uwekezaji mkubwa katika sekta ya Afya kwa kuboresha Miundombinu ya kutolea huduma lakini kuwekeza katika wataalam wa kutoa huduma yaani Madaktari Bingwa pamoja na Vifaa vya uchunguzi na ugunduzi wa magonjwa mbalimbali”.

“Uwepo wa miundombinu hiyo inaenda sambamba na kutafsiriwa na wananchi ambao wanapata huduma katika Vituo vyetu vya kutolea huduma. Kwa mantiki hiyo Wizara ya Afya imeweka kipaumbele kikubwa kuhakikisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi zinawafikia wananchi karibu na maeneo yao.Lengo la kambi hizi za utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi ni kuhakiksha wananchi wanapata huduma ,pia kuwapunguzia gharama za kusafiri kwenda katika Hospitali zetu za Kanda,Hospitali yetu ya Taifa na Hospitali maalum”.

“Tuna kambi sita zimeandaliwa ambazo zitaendelea kufanyika kwa nyakati nyakati tofauti kwa muda wa wiki mbili tumeanza na kambi 3 na nyingine 3 zitafuata baada ya hizi kuwa zimemalizika. Tuna kambi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga,Geita,Ruvuma,Lindi,Kigoma na Morogoro. Katika kambi hizi 3 tumefanikiwa kuona wagonjwa 3744 kati yao wapo wagonjwa 70 waliofanyiwa upasuaji,kadhaa wameainishwa kupata huduma za ubingwa bobezi kwahiyo wale wote tunaodhani wanahitaji huduma za ubobezi zaidi wao pia tutawaona katika Hospitali zetu za huduma bobezi mfano JKCI, na lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma zenye ubora”.

Mratibu wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya ambaye pia ni Mlezi wa Hospitali ya Bombo Dkt. Alex Magufwa amesema “Kambi hii imekuwa na mafanikio makubwa ambapo mpaka kifikia siku ya jana tumeona jumla ya wagonjwa 1945 na oparesheni 20 zimefanyika; oparesheni 7 ni magonjwa ya jumla,3 akina mama wenye uvimbe,3 mifupa 6 Magonjwa Masikio,Pua na Koo na 1 oparesheni ya kibofu,. Pia tumetoa Rufaa 14 ambazo ni matokeo ya Kambi hii ambapo wagonjwa 9 wamegundulika kuwa na changamoto katika moyo na wanahitaji upasuaji hivyo tumewapeleka kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI),1 saratani kwenye taasisi ya Ocean Road na wengine tumewapeleka Muhimbili”.

“Kambi hii imekuwa nzuri na muitikio umekuwa ni mkubwa na Madaktari wanajituma sana katika kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi”.