Wasiliana nasi | FAQ | Mails | Malalamiko |

Tanga Regional Referral Hospital
(Bombo Hospital)

BOMBO WAZINDUA KLINIKI YA MAGONJWA YA DAMU

Posted on: November 15th, 2024

BOMBO WAZINDUA KLINIKI YA MAGONJWA YA DAMU

Mapema leo Novemba 18,2024 Timu ya wataalam kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wamezindua Kliniki ya Hemophilia na Sikoseli katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ambayo imefadhiliwa na mdau Novo Nordisk Haemophilia Foundation ikiwa na lengo la kuongeza kasi ya upatikanaji wa dawa na matibabu kwa magonjwa ya damu Hospitalini hapo.

Hafla ya uzinduzi wa Kliniki hiyo umeongozwa na Dkt. Asteria Mpoto Mratibu wa Sikoseli na Hemophila kutoka Wizara ya Afya pamoja na Dkt. John Rwegasha Mratibu na Msimamizi wa Mradi Kitaifa na Mkurugenzi wa Idara ya Tiba kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili,Dkt. Frank Shega ambaye ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo pamoja na wauguzi kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Tanga zikiwemo Pangani,Kilindi,Korogwe,Muheza na Mkinga.

Uzinduzi wa Kliniki hiyo umeenda sambamba na mafunzo yaliyoratibiwa na mdau Norvo Nordisk Haemophilia Foundation (NNHF),Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pamoja na Haemophilia Society of Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Afya nchini yametolewa na wataalam wabobezi katika Magonjwa ya damu hususani Sikoseli na Hemophilia kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupitia Mradi wa kuongeza kasi ya Upatikanaji wa Huduma za Magonjwa ya Damu (Expanding Access to Blood Disorder Care Tanzania Chapter). Mafunzo hayo ambayo yamehusisha wataalam mbalimbali wa Afya katika Hospitali ya Bombo na wauguzi kutoka Hospitali za wilaya Mkoani humo ili kuwapatia elimu na uzoefu katika kuwahudumia wagonjwa wenye changamoto za magonjwa ya damu.

Aidha, Uzinduzi wa huduma hizo katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo umefanyika ambapo Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Frank Shega pamoja na kuwashukuru wataalam hao waliofika kutoa huduma ya kliniki ya sikoseli, amesema hii ni fursa adhimu kwa Wananchi na wakazi wa Mkoa wa Tanga kufika Hospitalini hapo ili kupata huduma hiyo na kwamba baada ya uzinduzi huo kliniki itakuwa mkombozi kwa Watanzania wenzetu wenye changamoto ya Sikoseli na Magonjwa mengine ya damu kufika Hospitalini hapa kufanya uchunguzi wa kina wa changamoto zao.