BOMBO WAZINDUA JENGO LA KITUO JUMUISHI KWA MANUSURA WA UKATILI WA KIJINSIA.
Posted on: December 16th, 2024BOMBO WAZINDUA JENGO LA KITUO JUMUISHI KWA MANUSURA WA UKATILI WA KIJINSIA.
Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bi. Pili Mnyema kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga amezindua rasmi Jengo la Kituo Jumuishi cha kutolea huduma kwa manusura wa Ukatili wa Kijinsia (ONE STOP CENTER) kwa Wanawake na Watoto waliofanyiwa ukatili wa kijinsia katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo.
Uzinduzi wa kituo hicho umefanyika wakati Katibu Tawala huyo akiikabidhi Menejimenti ya Hospitali ya Bombo Jengo hilo ambalo lipo tayari kwa Iengo la kusaidia wahanga wote wanaoteseka na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambao hawana sehemu faragha ya kukimbilia kwa ajili ya kueleza matatizo yao.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bi. Pili Mnyema ambaye ndiye mgeni rasmi amesema kuwa ni jambo zuri kuanzisha sehemu maalumu za kutoa huduma kama hizo katika jamii ili kuwasaidia walengwa wa majanga hayo kufika mahali ambapo wataweza kuzungumza kwa uhuru bila kuhofia.
Amesema " Kituo hiki kitakuwa huru kuhudumia wahanga wa ukatili wa kijinsia hasa akina mama na watoto ambao wao mara nyingi ndio wahanga huku wakiogopa kwenda hospitalini na kwenye vyombo vya usalama kutoa taarifa juu ya ukatili ambao wanafanyiwa na wenza wao au watu wao wa karibu wakihofia sehemu wanayokwenda kueleza matatizo yao hayako faragha kwao".
Aidha, Bi. Mnyema amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya wameliona hilo kuwa ni tatizo ndio maana wamefungua kituo hiki kwa fedha za Serikali kwa ajili ya kusaidia jamii kwa ujumla kuondokana na visa vingi vya matukio ya ukatili wa kijinsia ambao unadhoofisha maendeleo na ustawi wa Taifa letu".
Pia, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Bombo Dkt. Frank Shega ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kusaidia fedha kwa ajili ya upatikanaji wa Jengo hilo la One Stop Center pamoja na Shirika lisilo la kiserikali la GIZ kwa ushirikiano wao katika kurahisisha utendaji wa kazi kuwa mzuri kwani huduma zote zilizokuwa changamoto kwa manusura wa Ukatili wa Kijinsia zitapatikana hapo bila usumbufu huku kesi zote zikishughulikiwa kwa wakati".