Wasiliana nasi | FAQ | Mails | Malalamiko |

Tanga Regional Referral Hospital
(Bombo Hospital)

WATUMISHI WA BOMBO WAPATIWA MAFUNZO YA MAADILI.

Posted on: April 22nd, 2026

WATUMISHI WA BOMBO  WAPATIWA MAFUNZO YA MAADILI.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo, Dkt. Frank Shega, leo Aprili 22, 2026, amefungua rasmi mafunzo ya siku mbili kuhusu Kanuni,taratibu na Maadili ya Utumishi wa Umma kwa watumishi wa hospitali huku  yakilenga kuimarisha utendaji kazi na ubora wa huduma za afya.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Dkt. Shega amesisitiza umuhimu wa watumishi kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo, akibainisha kuwa uelewa wa kina wa maadili ya utumishi wa umma ni msingi muhimu katika kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji wa hali ya juu.

Mafunzo hayo yameendeshwa na Maafisa Maadili kutoka Ofisi ya Sekretarieti ya Utumishi wa Umma Kanda ya Mashariki, Jacquiline Msumba na Nadhha Msala ambao wameeleza kuwa maadili ya utumishi wa umma ndiyo dira inayowaongoza watumishi katika mwenendo na tabia njema kazini, jambo linalochangia utoaji wa huduma bora na matokeo chanya kwa jamii.

Aidha,Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa watumishi, na hatimaye kuinua kiwango cha huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga na maeneo jirani.