MAFUNZO YA MAADILI YAFUNGWA HOSPITALI YA BOMBO.
Posted on: April 24th, 2026Mafunzo ya siku mbili kuhusu kanuni, taratibu na maadili ya Utumishi wa Umma kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo yamehitimishwa rasmi Aprili 23, 2026, Katika Ukumbi wa Chuo cha Afya Bombo jijini Tanga.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na uongozi wa hospitali kwa kushirikiana na Maafisa Maadili kutoka Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Utumishi wa Umma Kanda ya Mashariki, yamelenga kuwakumbusha watumishi misingi ya mwenendo bora kazini ili kuongeza uwajibikaji, uadilifu na ubora wa huduma za afya kwa wananchi.
Wakufunzi, Jacquiline Msumba na Nadhha Msala, wamewahimiza watumishi kuzingatia maadili ya kazi kwa vitendo na kuepuka mienendo isiyofaa inayoweza kudhoofisha utoaji wa huduma bora.
Aidha, wamesisitiza kuwa maadili si chaguo bali ni wajibu unaojenga imani ya jamii kwa sekta ya afya.
Kupitia mafunzo haya, watumishi wanatarajiwa kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya kwa kuhakikisha huduma zinazotolewa zinazingatia viwango vya taaluma, utu na uwajibikaji wa hali ya juu.



