MAFUNZO YA MAADILI KWA UONGOZI YAFUNGWA BOMBO-TANGA
Posted on: April 24th, 2026Chuo Kikuu Huria cha Tanzania(OUT), kimehitimisha mafunzo ya siku tano ya Maadili ya uongozi,Uzingatiaji wa sheria na uwajibikaji kwa viongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa New Kiboko uliopo jijini Tanga kuanzia Aprili 20 na kutamatika leo Aprili 24, 2026.
Mafunzo hayo yaliyoshirikisha wajumbe wa Timu ya Usimamizi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo wakiwemo Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Timu ya Usimamizi wa Afya Mkoa,yameendeshwa na Wataalam kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na yalijikita katika masuala ya utawala na uongozi, usimamizi wa sheria katika kutoa huduma za afya pamoja na uongozi wa kuleta mabadiliko na usimamizi bora wa rasilimaliwatu.
Akihitimisha mafunzo hayo,Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo Dkt. Frank Shega, ameushukuru Uongozi wa Chuo hicho kwa mafunzo hayo ambayo yanaenda sambamba na utekelezaji wa mpango mkakati wa Hospitali ambao umeweka kipaumbele katika utoaji wa mafunzo ya mara mara kwa Viongozi ili kuongeza uwezo wao katika masuala mbali mbali ya usimamizi wa Hospitali.
“Matarajio ya mafunzo haya ni kuleta mabadiliko chanya katika taasisi,hivyo viongozi wajifanyie tathmini kuona wapi kuna madhaifu na kuyarekebisha ili kufanya kazi itakayoacha alama kwa taasisi na jamii wanazoziongoza. Katika mafunzo haya tumejichotea maarifa makubwa kutoka kwa wataalam hawa bobezi, naamini viongozi wote tutakaporudi kwenye ofisi zetu kile tulichokipata hapa kitakuwa na maana sahihi kama tutakifanyia kazi ipasavyo,” amesema Dkt. Shega.
Katika mafunzo hayo pia Dkt. Shega amewatunuku vyeti wataalam wote walioshiriki kama kielelezo cha kuthibitisha ushiriki wao katika mafunzo hayo.



