DKT SHEGA AFUNGUA MAFUNZO YA 5S KAIZEN HOSPITALI YA BOMBO.
Posted on: March 10th, 2026Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo, Dkt. Frank Shega, leo Machi 10, 2026 amefungua rasmi mafunzo ya 5S KAIZEN kwa watumishi wa hospitali hii ambayo yanaratibiwa na Wizara ya Afya kwa lengo la kuongeza ufanisi na ubora wa huduma za afya.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Dkt. Shega amesema mfumo wa 5S KAIZEN unalenga kuboresha mazingira ya kazi kwa kuyafanya yawe yenye mpangilio mzuri, usalama pamoja na kurahisisha utendaji wa kazi kwa haraka.
Amesisitiza kuwa utekelezaji sahihi wa mafunzo hayo utasaidia watumishi kuongeza ubora wa huduma wanazozitoa kwa wagonjwa na kwamba watajenga utamaduni wa kupanga vizuri maeneo ya kazi, kutumia muda kwa ufanisi na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma katika mazingira yenye mpangilio.
Kwa upande wao, Katibu wa Hospitali anayeshughulikia Idara ya Ubora, Happines Msengi, pamoja na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani, Dkt. Zahra Nuhu, wamesema mafunzo hayo ni muhimu kwani yatasaidia kuwakumbusha watumishi misingi ya ubora kazini, kuongeza uwajibikaji na kuboresha mazingira ya utoaji huduma.



