WATAALAM BOMBO WAPATIWA ELIMU YA MAGONJWA YA MASIKIO, PUA NA KOO.
Posted on: August 13th, 2026Baadhi ya watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo leo, Agosti 13, 2026, wamepata fursa ya kuongezewa maarifa kuhusu magonjwa ya Masikio, Pua na Koo-ENT, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uwezo wa wataalam katika utambuzi wa changamoto hizo na utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa.
Elimu hiyo imetolewa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Masikio, Pua na Koo wa Hospitali ya Bombo, Dkt. Mohamed Sachedina, ambaye amesisitiza umuhimu wa wataalam wa afya kuwa na uelewa mpana wa namna ya kutambua na kushughulikia changamoto za magonjwa hayo, hususan katika hatua za awali kabla ya mgonjwa kupata huduma za kibingwa.
Dkt. Sachedina ameeleza pia namna sahihi ya kuwahudumia wagonjwa wenye changamoto za Masikio, Pua na Koo, akisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua stahiki za awali ili kupunguza uwezekano wa madhara na kuboresha matokeo ya matibabu.
Vilevile, ameisihi jamii kuacha kutumia njia zisizo salama katika kushughulikia changamoto za Masikio, Pua na Koo, ikiwemo tabia ya kuchokonoa masikio kwa kutumia vitu visivyofaa, jambo ambalo linaweza kusababisha madhara na kuongeza tatizo badala ya kulitatua.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo hutoa Kliniki ya Masikio, Pua na Koo-ENT kila Ijumaa hivyo Wananchi wenye changamoto zinazohusiana na maeneo hayo wanashauriwa kufika hospitalini kwa ajili ya uchunguzi na kupata huduma stahiki kutoka kwa wataalam.



