USISUBIRI CHANGAMOTO,TAFUTA HUDUMA ZA UTENGAMANO MAPEMA.
Posted on: September 10th, 2026Wananchi Mkoani Tanga wamehimizwa kujenga utaratibu wa kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupata huduma za Utengamano-Rehabilitation mapema, badala ya kusubiri hadi pale wanapokumbwa na changamoto kubwa za kiafya ndipo waanze kutafuta huduma hiyo.
Wito huo umetolewa leo, Septemba 10, 2026, na wataalam wa Idara ya Utengamano kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo, wakati wa wasilisho maalum la kutoa elimu kwa watumishi wenzao kuhusu umuhimu wa huduma za utengamano katika kuboresha afya na kurejesha uwezo wa mgonjwa katika maisha ya kila siku.
Mfiziotherapia Moses Kufikiri amesema kuwa bado jamii ina mtazamo wa kusubiri hadi pale mtu anapokumbwa na changamoto ya kiafya ndipo aanze kufuatilia huduma za utengamano, jambo ambalo linaweza kuchelewesha mchakato wa kurejesha uwezo wa mwili na kumwezesha mhusika kurejea katika shughuli zake za kawaida.
Aidha, wananchi wameaswa kuondokana na dhana kwamba huduma za utengamano ni kwa ajili ya watu wenye ulemavu pekee, kwani huduma hizo zinaweza kuwa sehemu muhimu ya mchakato wa matibabu na kupona kwa watu wenye changamoto mbalimbali za kiafya.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo hutoa huduma za Utengamano kila siku Jumatatu hadi Ijumaa hivyo kama kuna mwananchi ana changamoto anashauriwa kufika hospitalini hapa.



