UPUNGUFU WA NGUVU ZA KIUME.
Posted on: August 6th, 2026Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo leo Agosti 6,2026 wamepatiwa elimu kuhusu Upungufu wa nguvu za kiume kupitia mada iliyowasilishwa na Daktari Bingwa wa Mfumo wa Mkojo, Dkt. Joshua Jackson.
Akiwasilisha mada hiyo, Dkt. Joshua amesema kuwa upungufu wa nguvu za kiume ni miongoni mwa changamoto za Afya zinazowaathiri wanaume ambapo mwanaume anapoteza uwezo madhubuti wa kusimamisha uume na kushindwa kufanya vizuri tendo la ndoa.
Ameeleza kuwa tatizo hilo linaweza kusababishwa na sababu mbalimbali, ikiwemo shinikizo la juu la damu, kisukari, uzito uliozidi, msongo wa mawazo pamoja na baadhi ya mtindo wa maisha usiozingatia afya.
Aidha amewashauri wanaume wenye changamoto ya namna hiyo kufika hospitalini mapema kufanyiwa vipimo vya awali ili kubaini kama ana changamoto nyingine za kiafya ambazo zinaweza kusababisha hali hiyo na kupatiwa matibabu na kurudi kwenye hali yake ya awali.
Dkt. Joshua amefafanua kuwa matibabu hutegemea chanzo cha tatizo na yanaweza kujumuisha matumizi ya dawa za kumeza, sindano maalum zinazotolewa kwenye uume, au upasuaji wa kuweka kifaa tiba maalum kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo inaendelea kutoa elimu kwa watumishi na jamii ili kuongeza uelewa kuhusu kinga, utambuzi wa mapema na matibabu sahihi ya magonjwa mbalimbali.



