MKUU WA MKOA TANGA AWATEMBELEA MAJERUHI WA AJALI YA LUSHOTO KATIKA HOSPITALI YA BOMBO.
Posted on: August 20th, 2026Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Buriani, leo Agosti 20, 2026, amefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo kuwatembelea na kuwafariji majeruhi wa ajali ya gari iliyotokea Agosti 18, 2026, katika eneo la Vuga, wilayani Lushoto.
Katika ziara hiyo, Balozi Dkt. Batilda Buriani amewapa pole majeruhi hao na kuwahakikishia kuwa Serikali ipo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu, huku akiwaombea kuendelea kupata nafuu na kurejea katika hali zao za kawaida.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza kuwa Serikali itasimamia gharama zote za matibabu ya majeruhi hao, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuhakikisha wananchi waliopata madhara katika ajali hiyo wanapata huduma stahiki bila kikwazo cha gharama.
Balozi Dkt. Batilda alipokelewa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo, Dkt. Frank Shega, ambaye pamoja na kumpokea, alimweleza hali ya majeruhi na hatua zinazochukuliwa na Hospitali katika kuhakikisha wanapata matibabu na uangalizi unaohitajika.
Akizungumza kuhusu hali ya majeruhi hao, Dkt. Shega amesema majeruhi wanane wanaendelea vizuri na wanaendelea kupatiwa huduma za matibabu kulingana na mahitaji yao ya kiafya.
Amesema Hospitali itaendelea kutoa huduma zote stahiki kwa majeruhi hao, pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo yao, hadi watakapopata nafuu na kupona.
Ajali hiyo ilitokea Agosti 18, 2026, katika eneo la Vuga wilayani Lushoto, mkoani Tanga, baada ya basi dogo aina ya Toyota kuacha barabara na kutumbukia bondeni, na kusababisha Vifo vya watu watano Papo hapo.



