Wasiliana nasi | FAQ | Mails | Malalamiko |

Tanga Regional Referral Hospital
(Bombo Hospital)

KAMBI YA KIBINGWA LUSHOTO YAFUNGWA RASMI

Posted on: September 25th, 2026

Madaktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo leo, Septemba 25, 2026, wamekutana na watumishi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kwa ajili ya kutoa mrejesho kuhusu kambi ya huduma za kibingwa iliyofanyika katika hospitali hii kwa muda wa siku nne.

Kambi hiyo iliyoanza Septemba 22, 2026, imelenga kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi wa Wilaya ya Lushoto pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kitaalam kati ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo na Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto.

Katika kipindi cha kambi hiyo, wananchi wamepata fursa ya kufikiwa na huduma mbalimbali za kibingwa kutoka kwa wataalam wa Bombo, hatua iliyosaidia kupunguza ulazima wa wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo katika hospitali nyingine.

Mbali na kutoa huduma kwa wananchi, madaktari hao pia wameendelea kushirikiana na watumishi wa Hospitali ya Lushoto kupitia mijadala ya kitaalam, majadiliano ya wagonjwa na kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali ya utoaji huduma za afya.

Ushirikiano huo pia unalenga kujenga uwezo wa watumishi kupitia uhamishaji wa ujuzi na uzoefu wa kitaalam, sambamba na kuimarisha mfumo wa rufaa na ufuatiliaji wa wagonjwa wenye mahitaji ya huduma za kibingwa.

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo imeendelea kutekeleza jitihada za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi kupitia kambi maalum, ushirikiano na hospitali za halmashauri pamoja na matumizi ya wataalam wake katika kuimarisha huduma za afya katika Mkoa wa Tanga.