KAMATI YA SIASA YA CCM MKOA TANGA YATEMBELEA WODI BINAFSI HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA TANGA-BOMBO.
Posted on: August 3rd, 2026Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi-CCM Mkoa wa Tanga, Agosti 2, 2026, ilifanya ziara katika Wodi Binafsi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo, kujionea maendeleo na ubora wa huduma zinazotolewa.
Kamati hiyo ilipokelewa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali, Dkt. Frank Shega, ambaye aliieleza kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika kuboresha huduma za afya na mazingira ya kuwahudumia wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdallah, aliipongeza Hospitali ya Bombo kwa kuendelea kuwa kinara wa utoaji wa huduma bora za afya mkoani Tanga.
Amesema huduma zinazotolewa hospitalini hapa zinachangia kuwawezesha Watanzania kuwa na afya njema na hivyo kuongeza tija katika shughuli za maendeleo.
Kamati hiyo, iliyokuwa ikiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Buriani, ilieleza kuridhishwa na ubora wa huduma, mazingira ya kisasa pamoja na kiwango cha huduma zinazotolewa katika Wodi Binafsi.
Wodi Binafsi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo, iliyozinduliwa mwezi Novemba 2025, imeendelea kujijengea sifa kwa kutoa huduma za afya zenye viwango vya juu, huku pia ikiendelea kuwa sehemu muhimu ya kukuza utalii wa tiba nchini.



