BOMBO YAPOKEA MASHINE YA UCHUNGUZI WA MADHARA YA KISUKARI MACHONI.
Posted on: September 28th, 2026Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo leo Septemba 28, 2026, imepokea mashine maalum ya kuchunguza madhara ya kisukari kwenye macho-Diabetic Retinopathy kutoka Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania-TDA.
Mashine hiyo imepokelewa na Dkt. Husein Mangaa kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali,sambamba na wataalam kutoka Idara ya Magonjwa ya Kisukari na Idara ya Macho.
Akizungumza baada ya kupokea mashine hiyo, Dkt. Mangaa ameishukuru TDA kwa msaada huo, akieleza kuwa utaimarisha huduma za uchunguzi na utambuzi wa mapema wa madhara ya kisukari kwenye macho kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga huku amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Bombo na TDA.
Kwa upande wake, Meneja wa Mpango wa TDA, Dkt. Renatus Fabian, amesema msaada huo umelenga kuwawezesha wagonjwa wenye kisukari kupata huduma bora za uchunguzi wa macho, kutokana na madhara ya ugonjwa huo kuweza kuathiri uwezo wa kuona.
Baada ya mashine hiyo kufungwa, wataalam wa Bombo wamepatiwa mafunzo ya matumizi yake ambapo Daktari Bingwa wa Macho, Dkt. Husein Abbas Tayebji, amesema mashine hiyo itaongeza ufanisi wa uchunguzi na kusaidia wagonjwa kupata huduma kwa wakati, hivyo kupunguza hatari ya madhara makubwa yanayoweza kuathiri uwezo wa kuona.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha huduma za afya na kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga na maeneo jirani.



