BOMBO WAPATIWA MAFUNZO KUTOKA MUHIMBILI.
Posted on: July 31st, 2026Wakuu wa vitengo wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo Julai 30, 2026, wameanza mafunzo ya siku mbili yanayotolewa na wataalamu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-MNH, yakilenga kuimarisha uongozi, usimamizi na utendaji wa huduma za afya.
Mafunzo hayo yamefunguliwa rasmi na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo, Dkt. Frank Shega, na yanafanyika katika ukumbi wa Chuo cha Afya Tanga-CoHAS.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Dkt. Shega amewataka washiriki kuyatumia kikamilifu kwa kuongeza maarifa na ujuzi utakaowasaidia kuwa viongozi bora katika vitengo vyao na kuwawezesha kuwaongoza wenzao kwa ufanisi zaidi.
Amesisitiza kuwa uwekezaji katika mafunzo endelevu ni msingi muhimu wa kuboresha utendaji kazi, kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya zenye ubora unaostahili.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo inaendelea kuweka kipaumbele katika kujenga uwezo wa watumishi wake ili kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa jamii.



